WAZIRI BASHUNGWA AKABIDHI KAZI YA UJENZI WA MADARAJA KWA MAKANDARASI USHETU
Na. Emmanuel Shomary
Ushetu DC
November 30, 2024.
WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kukagua na kukabidhi ujenzi wa madaraja kwa makandarasi.
Ziara hiyo imefanyika leo Novemba 30, 2024, ambapo Waziri Bashungwa amesema Rais Samia ametenga kiasi cha shilingi bilioni 868 kwa ajili ya kukarabati miundombinu iliyoathiriwa na mvua za El Nino na kimbunga Hidaya kama vile barabara na madaraja.
Bashungwa amesema Halmashauri ya Ushetu imetengewa shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya kukarabati madaraja manne yaliyoharibiwa na mvua, likiwemo daraja linalounganisha Ushetu na Geita.
Bashungwa amefafanua kuwa Halmashauri ya Ushetu inatekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja matatu yenye thamani ya shilingi bilioni 13.5 ambayo yatakamilika katika kipindi cha miezi 12, Pia daraja linalounganisha Ushetu na Geita lenye urefu wa mita 50 linalogharimu shilingi bilioni 5.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja, akisema kuwa wananchi wa Ushetu walikuwa wakikumbwa na changamoto kubwa kutokana na hali mbaya ya miundombinu.
Mhe. Macha pia amesema kuwa Shughuli zote za maendeleo zinaunganishwa na ujenzi wa miundo mbinu ya barabara hivyo ataendelea kuwafatilia wakandarasi mpaka mirafi ikamilike, pia wananchi waitunze miradi hiyo na kuwa waaminifu kwa kulinda vifaa vyote vya ujenzi.
Aidha Macha amewaasa wananchi kulinda afya zao kwani UKIMWI upo na unauwa hivyo Miradi yote inayofanyika pasipo afya haiwezi kuwa kitu
Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, ameelezea furaha ya Wananchi, akisema kuwa Serikali imejibu kiu yao ya muda mrefu ya kujengwa kwa madaraja ambayo yatakuwa na manufaa makubwa katika shughuli za kiuchumi na usafiri.
Katika hatua nyingine, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Samweli Mwambungu, ametoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mikataba ya ujenzi wa madaraja hayo, akisema kuwa kazi zitakamilika ndani ya miezi 12 na madaraja yatakamilika kwa ubora.
Wakandarasi kutoka Kampuni ya Salum Motor Transport Limited, wanaotekeleza mradi wa daraja la Ubagwe, wameahidi kuwa mradi huo utazingatia viwango vya ubora na kukamilika kwa muda wa mkataba.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Ushetu bi. Martha Shija ameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto ya madaraja kwani walikuwa wanapata shida wakati wa masika ambapo barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na maji mengi hivyo ujenzi huo utarahisisha mawasiliano vijiji
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa