WAJASIRIAMALI USHETU WAELEZA WALIVYONUFAIKA NA MIKOPO YA ASILIMIA 10.
Na Ushetu DC, KAHAMA.
WAJASIRIAMALI wa Halmashauri ya Ushetu Mkoani Shinyanga, wameeleza namna walivyonufaika na Mikopo ya asilimia 10 isiyokuwa na riba kwa kuanzisha viwanda vidogo vya kuongeza thamani mazao ya nafaka huku soko lao kubwa likiwa ni shule za Msingi, Sekondari na Wafanyabiashara wanaopatikana kwenye maeneo yao.
Haya wameyabainisha leo tarehe 04 Machi 2024, kwenye hafla ya siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika kata ya Sabasabini Halmashauri hiyo.
Hafla hiyo iliyokwenda sambamba na uchangiaji wa fedha za ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto Zahanati ya Sabasabini ambapo jumla ya Sh.Milioni 6.482 na mifuko ya saruji 93 vilipatakana na kukabidhiwa kwa kamati ya ujenzi ya Zahati hiyo.
Mwenyekiti wa kikundi cha Mpunze Industry, kilichopo kata ya Mpunze bi. Therezia Sita alisema, mwaka 2022 walipokea mikopo wa Sh.milioni 100 kutoka Halmashauri ya Ushetu, kati ya hizo Sh.milioni 35 walinunua mashine ya kukoboa na kusaga nafaka, kujenga kiwanda kidogo na kiasi kingine walikitumia kununua nafaka.
Alisema, kikundi chao wanazalisha unga wa sembe kuanzia kilo 5, 10 na 25 na soko lao kubwa ni shule za Msingi na Sekondari zilipo maeneo jirani, Wananchi na baadhi ya Wafanyabiashara wa nafaka na faida wanayoptaa wanagawana na kiasi kingine hufanya marejesho kwenye Mkopo wao wa Asilimia 10 ili kuwapatia fursa wengine kukopa.
Naye Katibu wa Kikundi cha Mapinduzi ya Viwanda Kata ya Uyogo, bi. Hadija Jumanne alisema, wao walikopeshwa Sh.milioni 90, kati yake Sh.milioni 2.4 wakanunua kiwanja, Sh.milioni 50 wakajenga Kiwanda na Sh.milioni 25 wakanunua nafaka, na sasa wanagredi Mchele na uUnga kuanzia kilo 5, 10, 25 hadi 50.
Aliendelea kusema, Masoko yao yanapatikana katika jiji la Dar es salaamu, Mwanza, Mkoa wa Tabora na wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga kwa kupitia kwa Wajasiriamali wenzao, na hivi karibuni wamepewa elimu ya kutangaza bidhaa zao mtandaoni na wanajindaa kutangaza huko ili kuongeza soko lao.
Mwenyekiti wa Jukwa la Uwezeshaji Wanawake Mkoa wa Shinyanga Dr. Regina Malimi alisema, wamekuwa wakitoa elimu ya biashara kupitia majukwaa ya wanawake yaliyopo kila Halmashauri ili kuwawezesha kuwekeza kibiashara kupitia Mikopo ya Asilimia10 na sasa baadhi yao wameanza kutengeneza viwanda vidogo.
Katika hatua nyingine, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Ushetu bwana Morgan Mwita alisema, wamekuwa wakihamasisha jamii kuunda na kusajili vikundi vya wajasiriamali na pia kuvipatia elimu ya ujasirimali ili kuviwezesha kujikwamua kiuchumi, na kwasasa wanajumla ya vikundi vya wanawake 436 vilivyosajiliwa, ambapo Wanawake ni vikundi 291, Vijana 114 na Wenye Ulemavu ni 31.
Alisema, katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuvipatia mikopo isiyokuwa na riba, vikundi 52 vya wanawake vimepewa kiasi cha Sh.milioni 639.07 na wameendelea kufanya vema katika nyanja ya kiuchumi kwa kuanzisha ujasirimali mdogo na kati huku wengi wao wakianzisha viwanda vidogo vya nafaka.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa