21 oktoba,2025
Ushetu,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadij Kabojela, ametoa wito kwa watumishi wa Halmashauri kuendelea kuzingatia wajibu wao katika kutunza mazingira, kufanya mazoezi kwa ajili ya kuboresha afya zao, pamoja na kudumisha ushirikiano katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiutendaji.
Akizungumza katika kikao maalum cha watumishi kilichofanyika katika ofisi za Halmashauri, Bi. Kabojela ameeleza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mtumishi na ni msingi muhimu katika kuhakikisha jamii inapata huduma bora katika maeneo yote. Amesema kuwa mazingira safi yanachangia ustawi wa afya za wananchi na kupunguza gharama za kukabiliana na magonjwa yanayotokana na uchafu.
Katika kuhimiza afya bora kwa watumishi, Mkurugenzi amewataka kuendelea kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuongeza tija na ufanisi kazini. Alibainisha kuwa mazoezi sio tu yanaboresha afya, bali pia yanajenga nguvu ya mwili na kuongeza uwezo wa kufikiri, hivyo kuboresha utendaji wa majukumu ya kila siku.
Aidha, Bi. Kabojela amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na umoja miongoni mwa watumishi katika utekelezaji wa majukumu ya kijamii na kikazi. Amesema kuwa mshikamano na mawasiliano mazuri kati ya watumishi ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Halmashauri na kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.
Alihitimisha kwa kuwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na kufuata maadili ya utumishi wa umma ili kuimarisha maendeleo ya Halmashauri na jamii kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0767639345
Simu ya kiganjani: 0767639345
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa