Ushetu DC
25 Novemba, 2025
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, amefungua mafunzo ya siku moja kuhusu kilimo bora cha karanga yanayoendeshwa na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) – Naliendele, Mtwara.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Waliya – Ushetu na yamehudhuriwa na Maafisa Kilimo kutoka kata zote za Halmashauri ya Ushetu. Kupitia mafunzo hayo, washiriki wamefundishwa mbinu mbalimbali za uzalishaji bora wa karanga, ikiwa ni pamoja na:
Aina mbalimbali za mbegu bora za karanga zinazostahili kwa maeneo tofauti,
Utayarishaji sahihi wa mashamba kabla ya msimu wa kilimo,
Mbinu bora za upandaji wa mbegu za karanga ili kuongeza tija,
Utunzaji wa mazao shambani kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo,
Mbinu sahihi za uvunaji wa zao la karanga ili kupata mazao yenye ubora na mavuno mengi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bi. Hadija Kabojela ameishukuru TARI–Naliendele kwa kushirikiana na Halmashauri katika kutoa elimu yenye manufaa kwa Maafisa Kilimo, na amewataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo kikamilifu katika kuwahudumia wakulima.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa zao la karanga ili kuinua kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Halmashauri ya Ushetu.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za utafiti na maendeleo ya kilimo ili kuboresha uzalishaji na kuongeza kipato kwa jamii.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0767639345
Simu ya kiganjani: 0767639345
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa