Na Emmanuel Shomary
USHETU DC.
27 Juni, 2024
Vikundi vya Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, wametakiwa kurejesha kwa wakati fedha za mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani walizochukua ili na wengine wenye uhitaji wa kukopeshwa, waweze kukopeshwa fedha hizo.
Agizo hilo limetolewa na kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Julius MTATIRO wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani Ushetu, katika kujadili taarifa ya Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ambapo amewataka viongozi wa Halmashauriya hiyo kuwafatilia wote ambao bado mpaka sasa hawajarejesha fedha hizo ili na Wananchi wengine wanufaike na mikopo hiyo isiyokuwa na riba.
Naye, Kaimu Mweka hazina wa Halmashauri ya Ushetu, Ndugu Charles MATUBA, wakati akitoa taarifa ya Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, amesema mpaka sasa Halmashauri hiyo inadai mikopo hiyo kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na watu mwenye Ulemavu shilingi milioni 20 huku wakiweka utaratibu mzuri wa kukusanya mikopo hiyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Mhe. Gagi LALA amesema kuwa kurejeshwa kwa mikopo hiyo ni lazima na sio ombi.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa jimbo la Ushetu, Emmanuel CHEREHANI, amewataka Wananchi wanapokopa fedha hiyo waende kuizalisha na sio kufanyia starehe.
Hata hivyo, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CPA Yusuph MABWE, amesema kiini cha matatizo ya baadhi ya vikundi kutolipa mikopo hiyo, Ni kutokana na baadhi ya watoa mikopo kutozingatia taratibu na kanuni za utoaji wa mikopo hiyo ya 10%
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa