Ushetu DC
Septemba 25, 2025
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bw. Deus Kakulima, ameongoza zoezi la kugawa hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi wa vijiji vya Igunda na Butibu, Halmashauri ya wilaya ya Ushetu Mkoani Shinyanga.
Zoezi hilo limefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Igunda, ambapo zaidi ya wananchi 1,000 wamekabidhiwa hati 1,022 za kumilikishwa ardhi kisheria.
Katika zoezi hilo, wananchi 595 wa Kijiji cha Igunda walipokea hati zao, huku wananchi 427 wa Kijiji cha Butibu wakipatiwa hati hizo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bw. Kakulima alisema hati hizo zitasaidia wananchi kuwa wamiliki halali wa maeneo yao, kuongeza usalama wa umiliki, na kuzuia migogoro ya ardhi katika vijiji hivyo.
Zoezi hilo limewezeshwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anamiliki ardhi yake kwa mujibu wa sheria, ili iweze kuwa chachu ya maendeleo na kuepusha migogoro ya mara kwa mara inayotokana na umiliki holela wa ardhi,” alisema Bw. Kakulima.
Wananchi waliopokea hati hizo wameeleza kufurahia hatua hiyo wakisema itawawezesha kutumia ardhi yao kama dhamana katika taasisi za kifedha pamoja na kurithisha mali zao kwa usalama zaidi.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0767639345
Simu ya kiganjani: 0767639345
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa