Na. Ushetu Dc, KAHAMA.
SHIRIKA la Tanzania Health Promotion Support (THPS), leo 15 machi, 2024, limekamilisha ukarabati wa Kituo cha tiba na matunzo ya Virusi vya UKIMWI (VVU) ya Kituo cha Afya Bulungwa kilichopo Kata ya Bulungwa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Mkoani Shinyanga na kukabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Zoezi la ukarabati liligharimu jumla ya TZS. 204,468,950 (USD M81,787.58) ikiwa ni sehemu ya mradi wa Afya Hatua, unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S.CDC)
Kituo kiliimarishwa ili kuhakikisha Wananchi wengi zaidi katika Halmashauri ya Ushetu wanapata huduma bora za afya na matibabu na hii ni pamoja na kubomoa jengo, uashi, vyuma, kuezeka paa, mfumo wa kutupa maji ya mvua, milango na madirisha, finishes, samani, usafi wa mitambo, usambazaji wa maji. mabomba, mifereji ya maji taka na mfumo wa uingizaji hewa, vifaa vya mabomba na mfumo wa umeme.
Dk. Daniel Magesa, Mkuu wa Tawi la Huduma za Kliniki kutoka U.S.CDC Tanzania ameungana na Bw. George Anatory, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa THPS, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa THPS katika kukabidhi rasmi kituo hicho kilichofanyiwa ukarabati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed KABOJELA ambaye ni mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya kituo cha Afya Bulungwa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ushetu, watumishi wa Kituo cha Afya Bulungwa na watumishi wa THPS wakishuhudia tukio hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo Bi. Kabojela alitoa shukurani zake kwa msaada mkubwa unaotolewa na Serikali ya Marekani kupitia THPS katika kudhibiti janga la UKIMWI na kuokoa maisha ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu. Aliahidi kudumisha ushirikiano unaohitajika na CDC na THPS ili kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Kwa upande wake Dk. Magesa alieleza kuwa serikali ya Marekani inaitambua na kuipongeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI), viongozi wa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia kwa dhamira ya kuboresha matokeo ya afya nchini Tanzania. Alisisitiza kuwa kuongezeka kwa ushirikiano katika kinga, tiba na matunzo ya VVU na UKIMWI kutasaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya na VVU, huku akisema Serikali ya Marekani inatambua na kuunga mkono ahadi hii.
Katika hatua nyingine, Kituo hicho kipya kilichokarabatiwa, kinatarajiwa kuweka mazingira bora ya kutoa huduma za tiba na matunzo ya VVU na hivyo kusababisha ongezeko la watu wanaopata huduma katika kituo hicho.
Katika maelezo yake Bw.George Anatory, alisema shirika lake limejipanga kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha watanzania wote wanapata huduma bora za afya na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi Nchini.
Bw.Anatory, alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi na matengenezo ya kituo hicho ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora za tiba na matunzo ya VVU sambamba na kuhimiza ufuasi wa huduma za tiba ya ARV kwa wapokea huduma.
"Nina imani kuwa msaada tuliotoa utaboresha utoaji wa huduma za kinga, tiba na matunzo ya VVU, na kusaidia kuokoa maisha katika wilaya ya Ushetu na maeneo jirani", alisema.
Kuhusu THPS
Tanzania Health Promotion Support (THPS) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2011, chini ya Sheria ya asasi zisizo za kiserikali nambari 24 ya 2002.
THPS inafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar; Wizara ya Jinsia, Vijana, Wazee na Makundi Maalum; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU/UKIMWI; Kifua kikuu; kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto; huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana; mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa afya, na UVIKO-19.
Kuhusu mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021- Septemba, 2026)
Mradi huu unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya (Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga) na katika jamii (Kigoma, Pwani na Tanga). Huduma hizi ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wasichana balehe na wanawake wadogo katika mkoa wa Shinyanga.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa