Na. Emmanuel Shomary
Ushetu DC, Kahama.
14 Agosti, 2025
KAHAMA
Watumishi wa Afya katika kituo cha Afya Bulungwa wametakiwa kuhakikisha malipo yote ya wateja yanayofanyika yanatolewa Stakabadhi na fedha hizo kupelekwa benki na pia waweke daftari la mapato na Matumizi katika kituo hicho.
Rai hiyo imetolewa na na afisa wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Happiness Bilakwate wakati wakitoa mafunzo ya elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa watumishi wa afya katika kituo cha afya Bulungwa.
“Hakikisheni malipo yote ya wateja wenu yaani wagonjwa mnayatolea stakabadhi na hizo pesa mmezipeleke benki, hii itasaidia kuweka vitu wazi na kuhakikisha fedha za Serikali zinakuwa salama, Lakini pia hakikisheni mnaweka daftari la mapato na matumizi hapa kituoni” Amesema Bilakwate.
Aidha Bi.Bilakwate amewataka watumishi kutojihusisha kwa namna yoyote na rushwa,Uhuni,Ulevi na kutotumia Lugha chafu kwa wateja na wahakikishe wanakuwepo kazini muda wote wa kazi wanapohitajika na wahakikishe wanaweka matangazo ya kukataa rushwa eneo la kazi.
“Rushwa ni adui wa haki,hakikisheni hamjihusishi kwa namna yoyote na vitendo vya rushwa,Uhuni na ulevi.Lakini pia tumieni Lugha nzuri kwa wateja wenu hata kama umevurugwa na mambo yako nje ya ofisi ila ukija kazini tumia Lugha nzuri kwa wateja wako na huo ndio utumishi wa kweli.
Na pia wekeni matangazo ya kukataa rushwa eneo la kazi” Amesistiza Bi.Bilakwate.
Kwa Upande wake Mganga mkuu wa Halmashauri ya Ushetu Dkt.Athuman Matindo amehaidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yalitolewa na afisa wa TAKUKURU na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa mtumishi yeyote ambaye atakwenda kinyume na taratibu za utumishi wa Umma.
“Tunashukuru sana kwa maelekezo haya,sisi kama Idara ya Afya Halmashauri ya Ushetu tunahaidi kuyafanyia kazi maagizo yote na hatutosita kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote ambaye atakwenda kinyume na taratibu za utumishi wa Umma” Amesema Dkt.Matindo.
Taasisi ya Kuzuia na kupambana rushwa (TAKUKURU) Wilayani Kahama mkoani Shinyanga imekusudia kutokomeza vitendo vya Rushwa mahali pakazi hasa kwa Idara ya afya ambapo kumekuwa na malalamiko takrbani kwenye Halmashauri zote za wilaya ya Kahama.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0767639345
Simu ya kiganjani: 0767639345
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa