Na. Emmanuel Shomary
12 Agosti, 2025.
ELIMU juu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, iliyolenga kuwakumbusha madhara na uharibifu unaoweza kusababishwa na Rushwa mahali pakazi, imetolewa leo tarehe 12 Agosti, 2025 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hospitali ya Wilaya ya Ushetu.
Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Maafisa kutoka Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilayani Kahama, bi. Happiness Bilakwate na ndugu George Japhet.
Mafunzo hayo yalilenga kuwakumbusha watumishi wa Idara ya Afya, hasa wanaotoa huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Ushetu, kuepukana na Rushwa na kutenda haki huku wakizingatia maadili ya taaluma zao.
Akiongea wakati wa Mafunzo hayo, Bi. Happiness amewataka Watumishi hao kuwa waadilifu na wenye hofu ya Mungu, ili kuwahudumia Wananchi wanaohitaji huduma za Afya kwa haki na usawa.
" Kazi yenu ni zaidi ya wito, ni sawa sawa na utumishi wa Mungu, fikiria mzee anakuja kutibiwa, halafu unamwambia gharama za juu, kiasi kwamba mzee wa watu analazimika kuuza mifugo yake ili akidhi gharama za matibabu, hii ni mbaya sana" alisema bi. Happiness.
Kwa upande wake, bwana Goeorge yeye amewataka watumishi hao kuridhika na kipato halali wanachopewa na Serikali, kwani tamaa ya kutamani mafanikio ya haraka, ndiyo hupelekea kuomba Rushwa kwa wateja wao.
"Sheria ya utumishi wa Umma, haimzuii mtu kuwa na kipato cha ziada, muhimu ni kutokuathiri muda wa muajiri, tuwe watu wa kujiongeza kwenye vipato halali na turidhike navyo, na siyo kujikita katika kuwaumiza Wananchi". Amesema bwana George.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ushetu, Dr.Athuman Matindo, amwawaahidi maafisa hao wa TAKUKURU kusimamia vema maadili kwa watumishi hao wa Afya, na kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaokiuka Maadili ya utumishi wa Umma.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0767639345
Simu ya kiganjani: 0767639345
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa