“MRADI HUU WA STADI ZA MAISHA KWA WANAFUNZI, KWETU UMEKUJA KWA WAKATI SAHIHI SANA” - Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Ushetu.
Na Emmanuel Shomary
Ushetu DC
11 Juni, 2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu Bi. Hadija KABOJELA, amewashukuru sana Serikali ya Tanzania kwa Kusirikiana na Mdau CAMFED kwa kuleta Mradi wa Stadi za Maisha kwa Wanafunzi wa Sekondari katika Halmashauri ya Ushetu.
Hayo ameyasema leo 11 Juni, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku 2 yanayofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Ushetu na kuhudhuriwa na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Walezi pamoja na maafisa elimu ngazi ya Halmashauri.
“Kwetu sisi Mradi huu umekuja wakati sahihi sana, Ombi langu kwa washiriki wote, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu Walezi hakikisheni mradi huu unafanikiwa ili watoto wetu wapate ujuzi utakaowasaidia katika Maisha yao ya baadae.
Naamini kwa kushirikiana na CAMFED Tanzania, tunaweza kuchochea maendeleo ya jamii yetu” alisema bi. Kabojela.
Katika hatua nyingine, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Ushetu, ndugu Emmanuel Clement MALIMA, amewasisitizia walimu hao kuyafanyia kazi mafunzo hayo yanayotolewa na CAMFED ili kuweza kuondoa tatizo la watoto wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali.
“Niwaombe walimu, sisi ndio wadau wenye mradi huu, tuhakikishe tunashirikiana pamoja ili tumkomboe mtoto wa Ushetu katika suala la kushindwa kumaliza masomo yake” alisema Malima.
Awali akitambulisha mradi huo, Kiongozi wa mradi wa Stadi za Maisha kutoka CAMFED Bwana James Mussa Mnyeti, amewaomba washiriki wa mafunzo hayo kuupokea mradi huo kwa mikono miwili kwani umekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha maendeleo ya wanafunzi.
Mradi wa CAMFED unafanya kazi katika Nchi tano barani Afrika Ghana, Malawi, Tanzania, Zambia na Zimbabwe. Na kwa Tanzania ulianza mwaka 2006 na unafanya kazi katika Mikoa kumi, Shinyanga, Morogoro, Pwani, Tanga, Tabora, Singida, Dodoma, Mwanza, Iringa na Dar es salaamu.
Kwa mkoa wa Shinyanga CAMFED, Inafanya kazi kwenye Halmashauri nne, Ushetu, Kishapu, Msalala na Shinyanga DC.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa