Ushetu DC
19 Septemba, 2025.
KATIKA kikao kilichofanyika mapema leo tarehe 19/09/2025, kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo Hospitali ya Wilaya ya Ushetu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hajida Kabojela, ameongoza kikao cha majadiliano ya mkataba wa awali baina ya Halmashauri ya Ushetu na wawakilishi wa kampuni ya kimataifa ya SOLDEMCOM AGRO LTD juu ya uwekezaji wa biashara ya kaboni katika eneo la Msitu wa Mpunze, uliopo ndani ya Halmashuri ya Wilaya ya Ushetu.
Kikao hicho pia kiliwahusisha wakuu wa idara mbalimbali wa Halmashauri ya Ushetu, ambapo pande zote mbili zilijadili masuala ya msingi yanayohusu masharti na utekelezaji wa mkataba wa uwekezaji huo.
Biashara ya kaboni imeelezwa kuwa ni fursa muhimu kwa Halmashauri hiyo katika kulinda mazingira na kuendeleza uchumi wa kijamii, kupitia mapato yatakayopatikana kutokana na uhifadhi na uendelezaji wa msitu wa Mpunze.
Mkurugenzi Kabojela amesema kuwa mazungumzo hayo ni hatua ya mwanzo kuelekea ushirikiano wenye tija kati ya Halmashauri na SOLDEMCOM AGRO LTD, ambapo mkazo utawekwa katika uhifadhi endelevu wa mazingira pamoja na kuongeza kipato cha wananchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa kampuni ya SOLDEMCOM AGRO LTD, bwana Amani Hosea, amesema kampuni yao imejipanga kuwekeza kwa manufaa ya jamii na kusaidia kuimarisha shughuli za maendeleo kupitia mradi huo wa kaboni.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0767639345
Simu ya kiganjani: 0767639345
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa