MHE. MTATIRO AIPONGEZA HALMASHAURI YA WILAYA YA USHETU.
Na. Emmanuel Shomary, USHETU DC.
MUWAKILISHI wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Adv) ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kuandaa, kujibu, na kuwasilisha hoja zinazohusu Utekelezaji wa Mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo ilikuwa na jumla ya hoja 32 na 16 kati ha hizi zilikaguliwa na kufungwa, 15 zipo kwenye hatua ya utekelezaji huku 1 haijatekelezwa huku akimtaja Bi. Hadija Kabojela kama Mkurugenzi na mwanamama wa kuigwa kama mfano.
Mhe. Mtatiro ameyasema leo tarehe 27 Juni, 2024 katika Baraza Maalum la CAG ambapo pamoja na mambo mengine Mhe. Mtatiro amewapongeza sana Waheshimiwa Madiwani wote na kipekee kwa Waheshimiwa wanamama ambao wameonesha uwezo mkubwa sana wa kuchambua, kujenga na kupambania hoja kwa lengo la kuiletea maendeleo Ushetu, kutetea haki na mali za Wanaushetu tena kwa kutumia na kusoma Kabrasha kwa kujiamini, utulivu na uzalendo mkubwa zaidi.
"Kwa dhati kabisa naipongeza sana Ushetu DC kwa namna ambavyo mmeonesha uwezo mkubwa wa kuandaa, kujibu na kuwasilisha taarifa zenu zinazohusu mapendekezo ya CAG, pia waheshimiwa madiwani wote hasa wanamama, mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Gagi Lala, Mkurugenzi wa Ushetu Bi. Hadija Kabojela na watalaam hakika mnastahili pongezi hizi mmekuwa mfano wa kuigwa kulinganisha na Halmashauri nyingine ambazo nimepita na kuona utekelezaji wa hili," amesema Mhe. Mtatiro.
Ushetu inatajwa kuwa na hoja chache zaidi kulinganisha na Halmashauri nyingine hapai Shinyanga ambapo hoja za nyuma zilikuwa 78, zimejibiwa 70 na kubakia 8 ambazo zipo kwenye hatua ya utekelezaji jambo ambalo limepongezwa sana pia na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo ambaye amesema kuwa kipekee ameshuhudia mshikamamo mkubwa wa madiwani, Mhe. Mbunge na wataalam wakiongozwa na Mkurugenzi Bi. Hadija Kabojela.
Akiahirisha mkutano huu, Mhe. Gagi amesema kuwa anapokea pongezi hizi zote, maelekezo na ushauri uliotolewa wote na kwamba wanakwenda kuanza kutekeleza huku akisisitiza kuwa kwa kauli moja, baraza la madiwani linaazimia na kuelekeza kuwa wale wote wanaodaiwa kutokana na mkopo wa fedha za asilimia 10 za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao hawajalipa watafutwe na walipe fedha hizo ili Halmashauri iweze kuondokana na hoja za CAG na pia kwa kufanya hivyo kutawezesha na wengine kukopa na hivyo kuinua uchumi wa wananchi wa Ushetu.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa