KIASI CHA TSH.BILIONI 4.27 KUIMARISHA MAWASILIANO MKOANI SHINYANGA - MHE. NAPE.
Na. Emmanuel Shomary,
Ushetu DC
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, imegharamia zaidi ya shilingi Bilioni 4 ambazo zitatumika kuimarisha mawasiliano mkoani Shinyanga kwa kujenga minara 30 katika Kata 29 zenye jumla ya vijiji 83, ambapo takribani wakazi 421, 259 watanufaika, huku akisisitiza matumizi sahihi na yenye faida na siyo vinginevyo.
Mhe. Nape ameyasema haya leo tarehe 19 Julai, 2024 wakati wa Wasilisho la Taasisi mbalimbali lililofanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa mkoa, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Taasisi, kampuni za simu na wadau wa mawasiliano mkoani shinyanga.
"Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na mawasiliano ya simu, ambapo kwa mkoa huu wa shinyanga Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ikiwakilisha Serikali inayapatia makampuni ya simu kujenga minara 30 katika Kata 29 ambapo ndani yake kuna vijiji 83 na hivyo kuwanufaisha wakazi 421, 259 wa Mkoa wa Shinyanga, hili ni jambo kubwa sana na lenye kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mawasiliano kwa Wanashinyanga," amesema Mhe. Nape.
Kwa upande wake RC Macha amempongeza sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mawasiliano kwa Wanashinyanga na Tanzania kwa ujumla jambo ambalo linaimarisha ulinzi, kuongeza uchumi wetu.
Akiwa Shinyanga, Mhe. Nape amezindua mnara wa Kampuni ya Halotel uliojengwa katika Kata ya Busangwa ambapo Serikali imetoa fedha zake za ruzuku shilingi Mil. 145, na ambapo wakazi zaidi ya 12,100 kutoka vijiji vya Mwanima, Mwajipungira, Pambe na Busangwa vyote vya Wilaya ya Kishapu watanufaika.
Kisha amemalizia kwa kukagua na kupongeza ujenzi mzuri na bora wa mnara wa Kampuni ya Honora uliopo Kata ya Bukomela, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu wenye uwezo wa 2G, 3G, 4G na 5G ambao utawanufaisha wakazi wa vijiji vitano (5) ikiwa ni zaidi ya lengo la awali la vijiji viwili (2) na kuwafikia wakazi zaidi ya elfu ishirini.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa