Na. Emmanuel Shomary,
Ushetu DC.
Jamii katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imetakiwa kuachana na imani potofu zinazochangia uwepo wa unyonyeshaji duni hali inayosababisha utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi ambaye ni diwani wa Kata ya Uyogo, Joseph Bundala akimuwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hadija Kabojela katika kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji yaliyofanyika leo Agosti 7, 2024, ambapo amewataka wataalumu wa afya kuwasaidia wakina mama kwa kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kunyonyesha watoto ili kuodokna na udumavu wa akili na mwili.
"Jukumu la kufanikisha unyonyeshaji unaofaa ni letu sote tukianza kwa kuacha imani potofu pamoja na kuweka mazingira yanayotoa usaidizi katika kipindi chote cha unyonyeshaji" amesisitiza Bundala.
Awali, akisoma taarifa kwa mgeni rasmi, Afisa lishe wa Halmashauri ya Ushetu, bi. Hadija Nassibu, amesema katika tafiti walizozifanya hivi karibuni wamebaini kuwa kati ya watoto kumi ni watoto wanne mpaka watano wanaonyonyeshwa ipasavyo na hii ni kutokana na uwepo wa imani potofu kwa baadhi ya jamii, na mtindo wa maisha.
"Kuna baadhi ya wanawake wanadai wanaponyonyesha maziwa yao hulala na kudondoka hasa wale wa chuchu saa sita lakini hapana, kinachochangia hayo ni maumbile ambayo wamewekwa na Mungu" amesema Khadija.
Kwa upande wao, baadhi ya akina mama wa Halmashauri ya Ushetu, wakizungumza baada ya maadhimisho hayo kwa nyakati tofauti, wamesema vijana wa siku hizi hawazingati taratibu za afya ya uzazi hali inayosababisha watoto kupata udumavu, kwa kutokunyonyeshwa kwa kipindi cha miaka miwili na pasipo kulishwa vyakula vya makundi yote pamoja na kuhofia madiliko ya miili yao.
Hata hivyo, kutokana na matokea ya utafiti wa afya ya uzazi yaliofanyika mwaka 2024 Kitaifa, imebainika kuwa watoto walionyonyeshwa maziwa ya mama pekee chini ya umri wa miezi sita ni asilimia 64, huku utafiti huo ukionyesha kuwa watoto walionyonyeshwa kwa miaka miwili ni asilimia 37%.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa