Na. Emmanuel Shomary,
Ushetu DC
Alhamis, 24 Julai, 2025.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga, imeshika nafasi ya tatu (3) Kitaifa katika viashiria vya utoaji wa huduma bora za afya.
Haya yamesemwa leo tarehe 24 Julai, 2025 na Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo
Dkt. Athuman Yusuph Matindo, wakati wa Kikao kazi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hospitali ya Wilaya ya Ushetu na kuhudhuriwa na Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, CHMT yote ya Ushetu, pamoja Waganga wafawidhi wote kutoka Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu.
Akisoma taarifa ya Utoaji wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kwa Mgeni rasmi, Dkt. Matindo alisema, Divisheni imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kuboresha Huduma za Afya, ikiwa ni pamoja na Upatikanaji wa Dawa Muhimu, Vifaa tiba na Vitendanishi kwa kiwango cha 95.6% kutoka 86.2% ya mwaka 2023/2024.
Katika hatua nyingine, Dkt. Matindo ameeleza kuwa, Divisheni imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa Mapato kutoka Tsh. 400 milioni, iliyokuwa bajeti ya mwaka 2024/2025 na kukusanya kiasi cha Tsh. 1.04 bilioni, ikiwa ni ongezeko la 210% ya lengo lake la ukusanyaji wa Makusanyo ya Uchangiaji wa huduma kwa mwaka husika.
"Ndugu Mkurugenzi, Divisheni imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika ukusanyaji wa makusanyo ya kuchangia huduma za Afya, hali hiyo pamoja na mengine mengi, yamepelekea Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu kushika nafasi ya tatu Kitaifa katika Viashiria vya Utoaji Huduma bora", alieleza Dkt. Matindo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Bi. Kabojela, amepongeza sana juhudi hizo na kuahidi kuendelea kushirikiana vema na Divisheni hiyo ili kuboresha zaidi Huduma za Afya Ushetu.
" Nimefurahi sana kwa mafanikio haya makubwa mmepata kama Divisheni na Halmashauri kwa ujumla, mm ninaahidi kuendelea kushirikana na ninyi kwa ukaribu zaidi kwa kila hatua, ili kuleta ufanisi wa utoaji bora wa huduma za Afya ndani ya Halmashauri yetu", alisema Bi. Kabojela.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, inajumla ya Zahanati 32, Vituo vya Afya 5 na Hospitali 1, huku ikiwa na jumla ya watumishi 365 wa ajira za kudumu na watumishi 84 wa ajira za Mkataba, idaidi hii ya watumishi waliopo ni sawa na 70% ya mahitaji halisi.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa