“USHETU MENIPOKEA VIBAYA, NA NIMECHUKIA.” RC Shinyanga.
Maneno hayo yamesemwa leo Machi 30, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Christina Mdeme alipofika Makao makuu ya Halmashauri ya Ushetu yaliyopo katika Kijiji cha Nyamilangano na Kata ya Nyamilangano.
Mh. Mdeme ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya Kamati ya siasa ya Mkoa kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya UShetu.
Katika kikao hicho na watumishi wa Halmashauri ya Ushetu kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hospitali ya Wilaya ya Ushetu, Mh. Mdeme ameelezea masikitiko yake kwa jinsi alivyopokea Matokeo ya Hati chafu kwa Halmashauri ya Ushetu.
“Kwa kweli hili halikubaliki, haiwezekana hata kidogo Ushetu pekee yenu mpate hati chafu, kama wenzenu Nchi nzima wamepata hati safi, kwanini ninyi pekeyenu?” alihoji Mh. Mdeme.
Katika hatua nyingine, Mh. Mdeme aliendelea kutoa maagizo, “Ushetu mnashida nyingi sana, Ugavi kila mara ni Inflation, bei zinapandishwa tu, vitu vinaonekana gharama zipo juu, achene tabia hizo.
Mfumo wa mapato unachezewa, POS pia zimechezewa, hili ni tatizo, mimi nataka Ushetu mbadilike na kama kuna mtu anahisi hawezi kubadilika, basi atupishe mapema sana.
Tutasimamia matumizi mazuri ya fedha za Umma, tuliahidi kwenye ilani yetu ya CCM.
Naagiza mpandishe mapato ya Halmashauri, ikiwemo kubuni vyanzo vipya vya mapato, Mfano tunaweza kulima Mkonge huku kwetu ikawa mojawapo ya mazao ya biashara Ushetu, Pia tunahitaji walau Hekari 100 kwa ajili ya kilimo cha Matunda, soko lipo na kiwanda cha Jambo kipo na kinatengeneza juisi.
Lakini pia Watumishi wa Ushetu hamna Mahusiano mazuri kazini, watu hawasemeshani maofisini, Wakuu wa Idara na Vitengo, embu tengenezeni mahusiano mazuri na watu wenu, pakiwa na mahusiano mazuri kazini, hata kazi zenu zitakuwa njema na mtaleta huduma bora pia kwa Wananchi wetu.
Sekta ya afya lazima iboreshwe, ikiwemo Madirisha ya Wazee, dawa kwa ajili ya wazee na Daktari pia kwa ajili ya wazee. Tunahitaji uwepo wa dawa na huduma bora kwa wazee wetu.
DMO, nakuagiza fuatilia, Bulungwa na Kijiji cha Mseki pana shida, wizi wa madawa upo sana, dawa zinapotea, Nakuagiza ukasimamie haya kwa Uaminifu mkubwa sana, dawa na vifaa tiba visipotee.
Naomba sana tubadilike katika utendaji kazi. Kila mtu ajitume na afanye kazi kwa kuzingatia maelekezo na taratibu za Utumishi wa Umma.
Watumishi wote tunawajibu wa Kusimamia maadili ya Watoto, Maadili yanaanzia nyumbani, ni lazima sote tusimamie hayo kwa Uaminifu. Ubakaji na mauaji havina Afya tena, ni lazima tushurikiane na Jeshi la Polisi katika kupinga na kuzuia haya lakini pia kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Ushetu nitarudi, lazima nitarudi, Asanteni,” Alisema Mh. Mdeme.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa