"NIWATAKE WANAWAKE WENZANGU NA JAMII YOTE MKOA WA SHINYANGA KUPINGA UKATILI KWA VITENDO" - RC MNDEME
Na. Ushetu DC.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewataka wanawake wote na jamii kwa ujumla kuendelea kupinga, kukemea na kupambana dhidi ya ukatili wa kijinsia katika maeneo wanayoishi au kufanyia shughuli zao, kwa kuwa tatizo hili bado lipo miongoni mwa jamii zinazotuzunguka.
RC Mndeme ameyasema hayo leo tarehe 8 Machi, 2024 wakati akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, sherehe iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Manispaa ya Shinyanga ambapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vikundi vya wanawake, viomgozi wa Vyama na Dini huku akisisitiza kuwa jitihada za kuondoa ukatili huu zinapaswa kuanza na jamii yenyewe.
"Tunapoadhimisha Siku hii ya Wanawake Duniani, niwatake sote kwa pamoja kuendelea kupinga, kukemea na kupambana dhidi ya ukatili wa kijinsia ambao bado upo miongoni mwetu na jamii zinazotuzunguuka, kwa kuwa juhudi hizi tunapaswa kuanza nazo sisi wenyewe, ukizingatia wanaotenda haya matukio tunaishi nao," amesema RC Mndeme..
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita amesema kuwa, Wanawake wanaposherehekea siku ya leo, pamoja na mambo mengine lakini pia wanao wajibu wa kumsemea mema na mazuri yote anayoyafanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa ameendelea kuwatumikia vema Watanzania na kuwaletea maendeleo ya kweli.
Kando ya hayo, RC Mndeme amepokea zawadi na misaada mbalimbali kutoka kwa wadau wakiwemo Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Wakurugenzi wa Halmashauri na Taasisi, Vikundi , Shirika lisilo la Kiserikali, YAWE, Life Water International, Rafiki SDO,TCRS, ADD International na ICS.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa