Na Emmanuel Shomary, Ushetu DC.
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Ushetu Mkoani Shinyanga, limepitisha makadirio ya bajeti ya Sh.bilioni 41.2 kwa mwaka wa fedha ujao wa 2025/2026, huku likiwasisitiza wakulima wa mazao ya biashara kutotorosha mazao hayo ili kufikia lengo la makusanyo tarajiwa.
Aidha, limependekeza kupatiwa watumishi wapya 436 na watumishi 697 kupandishwa vyeo au madaraja na 19 kubadilishiwa madaraja yao.
Bajeti hiyo imepitishwa leo Feb 4,2025 katika kikao cha baraza la Madiwani la Halmashauri ya Ushetu na kuipongeza Serikali kwa kuendelea kuwapatia fedha za ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ile iliyoanzishwa kwa nguvu za Wananchi kwenye sekta ya Afya na Elimu.
Akisoma makadirio hayo ya bajeti, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo bwana Shigela Ganja alisema, bajeti hiyo imeongezeka kulinganisha na mwaka unaendelea wa 2024/25 ambapo waliweka makadirio ya kukusanya na kutumia Sh.bilioni 35.5 ikiwemo mapato lindwa na yasiyolindwa.
Bwana Ganja alisema, mwaka wa fedha 2025/2026 wanatarajia kukusanya kiasi cha Sh.bilioni 41.2, huku mapato ya ndani yasiyolindwa ni Sh.bilioni 3.85, miradi ya maendeleo Sh.bilioni 1.5, matumizi menginenyo Sh.bilioni 2.3, Ruzuku ya Mishahara Sh.bilioni 25.6, Ruzuku ya Miradi Sh.bilioni 9.36, Ruzuku ya Serikali Sh.bilioni 4.6 pamoja na fedha kutoka kwa Wananchi Sh.bilioni 4.6.
Naye diwani wa viti maalumu wa kata ya Bulungwa bi. Ester Matone alisema,ili kufikia malengo hayo ni vema Halmashauri ikaendelea kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vilivyopo kwani asilimia kubwa ya mapato yake yanatokana na zao la tumbaku kulinganisha na mazao mengine ya biashara.
Katika hatua nyingine, Diwani wa kata ya Nyamilangano, mh. Robert Mihayo alisema, utoroshaji wa mazao na kwenda kuuzwa kinyemela utasababisha kutokufikia malengo hivyo kila Diwani kwenye eneo lake ahakikishe analisimamia hili ili kufikia lengo la makusanyo kwa zaidi ya asilimia 100 kama ilivyotokea mwaka uliopita wa 2023/2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Anuani: S. L. P 50 Kahama
Simu: 0759888848
Simu ya kiganjani: 0759888848
Barua pepe: ded@ushetudc.go.tz Tovuti www.ushetudc.go.tz
Hati Miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu . Haki zote zimehifadhiwa